Environmenatal Reporting Services at NEMC
Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC)
lilianzishwa kwa Sheria ya Mazingira (Sura ya 191) Kifungu cha 16 kama
taasisi ya serikali ya kuhifadhi na kusimamia mazingira. Madhumuni ya
kuanzishwa kwa Baraza kama yalivyoainishwa katika kifungu cha 17 cha
Sheria hiyo kinaainisha madhumuni ya kuanzishwa kwa Baraza kuwa ni
kuratibu utekelezaji wa sera na Sheria ya Mazingira katika maeneo makuu
manne:-
i) Uzingatiaji na usimamizi (enforcement and compliance) wa Sheria ya Mazingira,
ii) Usimamiaji mchakato wa Tathmini ya Athari kwa Mazingira (TAM)
(Kuratibu, kufanya mapitio ya ripoti za TAM kutoka kwa wenye miradi na
kufuatilia utekelezaji wake),
iii) Uratibu wa ushirikishwaji umma katika kufanya maamuzi yanayohusu masuala ya mazingira na;
iv) Kusimamia kwa ujumla na kuratibu masuala yote yanayohusu
mazingira kwa mujibu wa Sheria ya Mazingira na sheria nyingine zozote
zilizoandikwa.
Majukumu ya Baraza
Kifungu cha 18 (2) ya Sheria ya Usimamizi wa Mazingira kimeainisha majukumu ya Baraza kama ifuatavyo;
i) Kufanya uhakiki wa Mazingira (Environmental Audit);
ii) Kufanya tathmini ambazo zitasaidia katika kuhifadhi na kusimamia mazingira;
iii) Kufanya utafiti na kuratibu utafiti wa mazingira, kuchunguza,
kutathmini na kukusanya taarifa na matokeo ya utafiti na kuzisambaza kwa
wadau;
iv) Kufanya mapitio na kutoa mapendekezo ili kuwezesha kupitishwa kwa taarifa/ripoti za (TAM);
v) Kuainisha miradi au programu zinazohitajika kufanyiwa ukaguzi na ufuatiliaji (Audit and Monitoring);
vi) Kuhimiza na kuhakikisha usimamizi na uzingatiaji wa viwango vya taifa katika utekelezaji wa sheria.
vii) Kuanzisha hatua madhubuti zenye lengo la kulinda na kudhibiti
ajali zinazoweza kusababisha uharibifu wa mazingira na kubuni njia za
kurekebisha maeneo ambayo yamepata uharibifu;
viii) Kutekeleza programu zenye lengo la kutoa elimu ya mazingira na
kukuza weledi kwa kushirikiana na taasisi na sekta za wizara mbalimbali
kwa lengo la kuhakikisha usimamizi madhubuti na ushiriki wa jamii katika
shughuli za kuhifadhi mazingira;
ix) Kuanzisha na kuendeleza mfumo wa kuandaa na kusambaza taarifa za mazingira nchini;
x) Kuchapisha na kusambaza miongozo mbalimbali ya usimamizi wa mazingira inayolenga udhibiti wa uharibifu wa mazingira;
xi) Kutoa ushauri wa kitaalamu na kusaidia taasisi na asasi
mbalimbali zinazoshughulika na usimamizi wa maliasili na mazingira, na;
xii) Kufanya shughuli nyingine zozote kwa maagizo ya Waziri wa
Mazingira au kutokana na uhitaji wakati wa utekelezaji wa sheria ya
Mazingira.
Muundo wa Baraza
Ili kutekeleza majukumu yake kikamilifu Baraza limezigawa shughuli
zake za kila siku katika kurugenzi 5 na vitengo 4 kama ifuatavyo:-
i) Kurugenzi ya Uzingatiaji na Utekelezaji wa Sheria za Mazingira
(Directorate of Environmental Compliance and Enforcement – DECE);
ii) Kurugenzi ya Tathmini ya Athari kwa Mazingira (Directorate of Environmental Impact Assessment – DEIA);
iii) Kurugenzi ya Mipango ya Mazingira na Utafiti (Directorate of Environmental Planning and Research – DEPR);
iv) Kurugenzi ya Habari, Mawasiliano na Uhamasishaji (Directorate of
Environmental Information, Communication and Outreach – DEICO);
v) Kurugenzi ya Utawala na Fedha
vi) Kitengo cha Huduma za Sheria (Legal Services Unit);
vii) Kitengo cha Ukaguzi wa Mahesabu ya Ndani (Internal Audit Unit);
viii) Kitengo cha Mipango na Bajeti (Corporate Planning & Budget Unit – CPU);
ix) Kitengo cha Manunuzi na Ugavi (Procurement Management Unit – PMU).
Aidha, mpaka sasa Baraza lina ofisi 3 za kanda. Kanda hizo ni Nyanda
za Juu Kusini, Ziwa na Kaskazini na ofisi za kanda hizo ziko katika miji
ya Mbeya, Mwanza, na Arusha.
Taarifa ya utekelezaji wa kazi za Baraza kuanzia Julai 2005 hadi Machi 2010 itawekwa hapa hivi karibuni.